Hamkani si shwari tena. Wasemavyo Waswahili, akufukuzaye hakwambii toka. Tamko la Rais Uhuru Kenyatta hivi majuzi kwamba hajali ni nani atakayemrithi mwaka wa 2022 ni ishara tosha kwamba ufa kati yake na naibu wake William Ruto unazidi kupanuka na huenda stakabadhi ya kifo cha Jubilee ikatiwa saini kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Hata ingawa Ruto anajikakamua kutoa taswira kwamba wako pamoja na Uhuru, huku akijitaja kama mtu wa mkono wa rais, sura yake, lugha ya kimwili na matamshi ya wandani wake, zinaashiria ndoa baina ya wawili hawa ishavunjika na merekebu ya Jubilee yazidi kuzama.
Historia ya urithi
Tangu tulipojinyakulie uhuru, Kenya imekuwa na makamu wa rais wapatao kumi sasa lakini hawajabahatika kukalia kiti teule cha rais wa nchi. Labda hii imesababishwa na karata tata za siasa za urais, huku wachanganuzi wa kisiasa wakihoji ni kama kiti hiki kina mikosi au laana fulani.
READ MORE
Hope for Coast squatters as State settlement plan takes off
Ruto: Why I have no apologies for donating millions to the Church
President has left out the Meru people, Kiraitu claims
There is little for Kenyans to celebrate under Kenya Kwanza government
Punde tu kiongozi anapofi ka nambari mbili, siasa huchipuka, aghalabu siasa za kikabila, kimaeneo na hata kichama, huku mirengo mingine ikivunjwa na mingine kuundwa.
Mara nyingi, hii huwa ni njama na mikakati ya kumkwaza makamu wa rais kumrithi rais aliyeko mamlakani. Kuna msemo kwamba katika siasa, hakuna maadui na marafi ki wa kudumu ila tu maslahi.
Historia ya siasa ya urithi wa Jomo Kenyatta na sasa mwanawe Uhuru inaelekea kujirudia ingawa mirengo na misingi ya kisiasa imebadilika. Kwa upande mmoja, vita vya ubabe wa kisiasa baina ya Jomo na Jaramogi ulipekea viongozi hao wawili kwenda msamba na kuzika kabisa ndoto ya Odinga kuwa rais wa pili nchini.
Kwa sasa, kuna mwelekeo kwamba Uhuru hana nia ya ya kumtawaza naibu wake Ruto kuwa rais atakapostaafu.
Nitaangazia kwanza uhusiano baina ya Jomo na Jaramogi, kisha Uhuru na Ruto na kutamatisha na kudura ya makamu wa rais humu nchini tangu Kenya ijinyakulie uhuru mwaka 1963.
Chanda na pete
Kwa mujibu wa kitabu “The Reds and the Blacks” kilichoandikwa na aliyekuwa balozi wa kwanza wa Marekani Kenya baada ya uhuru, William Attwood, na ambacho kilipigwa marufuku humu nchini miaka ya hapo awali, Kenyatta alikutana na Jaramogi mara ya kwanza kwenye miaka ya 1950.
Wakati huo, Jaramogi alikuwa mfanyi biashara mashuhuri kwenye eneo la Ziwa Victoria ambaye alijiingiza kwa siasa kupitia kwa ushawishi wa Kenyatta.
Yadaiwa kwamba Kenyatta alikuwa na shukurani si haba kwa Jaramogi kwa kumkopesha pesa wakati wa harakati za kupigania uhuru na pia kwa kumpigania kutolewa kizuizini. Jaramogi pia alikuwa mstari wa mbele kumsaidia Kenyatta kuwa Waziri Mkuu wa kwanza na hatimaye rais wa kwanza wa jamhuri ya Kenya kwa kupigania ushindi wa chama cha Kanu mwaka wa 1963.
Yamkini Jaramogi alikuwa na kila sabab kutamani kumrithi Kenyatta kwani kibinadamu, Jomo alikuwa na deni la kumlipa mwandani wake huyu wa karibu. Akiwa na miaka yapata 50 (kama vile Ruto sa hii), Odinga alijihisi kuwa yeye ndiye aliyestahili kumrithi Jomo.
Hata katika hafl a na sherehe za kitaifa, Jaramogi alivalia mavazi ya kufanana na Jomo, ikiwemo kofi a mithili ya zile za kiislamu huku akibeba fi mbo ya manyoya (fl ywhisk). (Fananisha taswira hii na pale Uhuru na Ruto walipochukua uongozi huku wote wakivalia mashati meupe na tai nyekundu).
Mkono wa kushoto
Kwa mujibu wa Attwood, Jaramogi alikuwa mwanasiasa mkakamavu, na mwenye maono makubwa kwa siasa na maendeleo ya nchi ya Kenya. Haiba hii ilimfanya kuzivutia serikali za Urusi na Uchina, ambazo walimwona kama aliyefaa kumrithi Kenyatta ambaye nchi hizo zilianza kuhisi kwamba alikuwa anapoteza akili timamu kwa sababu ya uzee.
Hata hivyo, Jaramogi alikuwa na mapungufu yake, ikiwemo kiburi, kupenda sifa, tamaa ya uongozi na hasira za karibu. Yasemekana kwamba misaada ya kifedha na kisiasa aliyopokea kutoka Urusi na Uchina ilimfurisha kichwa Jaramogi hata kujiona alikuwa mkubwa kuliko Jomo.
“Jaramogi alikuwa mwanasiasa mwenye haiba ya juu na mvuto kwa watu wengi aliposimama kwenye jukwaa za kisiasa kando na kuwa na wafuasi wengi sugu hasa kutoka jamii yake ya Waluo,” asema Attwood.
Hii iliwafanya wandani wa Kenyatta kuhisi kwamba Jaramogi alikuwa akijijengea himaya yake kisiasa ndani ya chama cha Kanu.
Kidagaa kuoza
Dalili kwamba kidagaa kimeanza kumuozea Jaramogi zilijitokeza wakati Kenyatta alipokuwa safarini London kuhudhuria mkutano wa Jumuia za Madola.
Kabla ya kuondoka nchini, Kenyatta alimtawaza mmoja wa mawaziri wake, Joseph Murumbi, kuwa kaimu waziri mkuu (Linganisha na waziri Matiang’i kutawazwa kusimamia Baraza la Mawaziri).
Jaramogi na wafuasi wake walikerwa sana na tukio hili kwani waliona makamu wa rais amedhalilishwa. Jaramogi alikasirika na kukataa kuandamana na Kenyatta kwenda kwenye kiwanja ndege.
Tukio jingine ni wakari rais wa Zambia Kenneth Kaunda alipowasili humu nchini ambapo rais Kenyatta hakuandamana na makamu wake kumlaki Kaunda kama ilivyokuwa desturi ya itifaki. Wakati wa sherehe moja ya Umoja wa Mataifa, Kenyatta alimtuma mmoja wa mawaziri wake kumwakilisha.
Yadaiwa kwamba waziri huyu, wakati wa kusoma hotuba ya rais, hakutaja uwepo wa Makamu Rais Odinga aliyekuwa amehudhuria hafl a hiyo, kinyume kabisa na itifaki.
Ndoa kuvunjika
Hatimaye, uhusiano baina ya Jomo na Jaramogi ulivunjika kabisa wakati wa uchaguzi wa kitaifa wa chama cha Kanu mwaka 1966 ambapo wanachama walipiga kura kwa kauli moja kubadilisha katiba ya chama na kufutilia mbali nafasi ya naibu makamu wa rais wa chama (nafasi iliyotengewa Odinga)
Yadaiwa Jaramogi alipandwa na mori na kufululiza kutoka kwa mkutano huo wa chama cha Kanu na hatimaye kuanzisha chama cha kwanza cha upinzani, Kenya Peoples Union (KPU), jambo ambalo lilikuwa mithili ya uhaini wakati wa sera za chama kimoja cha kisiasa. Siku hizi, watu wanasema vindu vichechanga (mambo hubadilika).
Sasa tunapoangazia siasa za mwaka 2022 za kumrithi mtoto wa Jomo, Uhuru Kenyatta, taswira ni gani? Tayari kuna wandani wa Ruto ambao wanahisi naibu wa rais amedunishwa vya kutosha na Uhuru na lingekuwa jambo la busara iwapo Ruto na wandani wake wangehama Jubilee na kujiunga na upinzani.
Upinzani ndani
Lakini je, Ruto anayo haiba na misuli ya kuongoza upinzani? Ieleweke kwamba undugu baina ya Ruto na Uhuru ulianza wakati wiwili hawa waliposhitakiwa katika Mahakama ya Kitaifa ya Jinai (ICC) kuhusiana na machafuko ya kisiasa ya mwaka 2008/2009.
Kulikuwa na dhana kwamba kuchukua mamlaka kwa hawa wawili kungewapa nguvu za kuwawezesha kuepuka jinamizi la kesi ya ICC.
Hii ilivutia hisia kali kwa wapiga kura hasa wa maeneo ya Kati ya Kenya na Bonde la Ufa mbayo yana wingi wa kura humu nchini.
Kwa hivyo, wakati joto la kisiasa linapozidi kupanda kila kunapokucha, ni jambo la msingi kujiuliza kama kuna deni baina ya Ruto na Uhuru au Uhuru na Raila Odinga, mwana wa Jaramogi ambaye alimfaa Jomo si haba wakati wa mapambano ya kujinyakulia uhuru.