Wabunge 10 kutoka majimbo ya Kisii, Nyamira na Migori wamesema kuwa mswada wa punguza mizigo unaopigiwa Debe na Dkt Ekuru Aukot hautafanikiwa kwa maana una nia ya kuchukua mamlaka kutoka kwa Wakenya. Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kongamano la Wabunge wa Gusii Joash Nyamoko, wabunge waliokuwa wakizungumza wakati wa mchango wa makanisa 10 katika eneo bunge la Bonchari, Kisii walisema mswada huo haustahili kuwepo kwa sasa.
Nyamoko alisema kuwa Wakenya wanajivunia mfumo wa sasa ambapo kuna majimbo 47 na maeneo bunge 290 na kwamba hakuna jamii hata moja itakubali kuona maeneo yake ya utawala yakiondolewa kwa ajili ya manufaa ya kisiasa ya watu wachache.
“Hakuna mtu anaweza kutuambia kuwa Kenya itakuwa nchi bora iwapo tutapunguza majimbo na maeneo bunge kwa maana hiyo ni sawa na kuturejesha mahali tulipokuwa miaka 30 iliyopita ambapo ilikuwa vigumu kupata huduma karibu,” akasema Nyamoko.
Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro alisema kuwa Wakenya walikuwa na haja ya kuwa na barabara nzuri, hali bora ya afya, chakula cha kutosha, maji safi ya kutosha na haya yote hayawezi kupatikana iwapo tutapunguza maeneo ya uwakilishi.
READ MORE
Kenyans are politically overrepresented, says Ekuru Aukot
Gusii leaders oppose tribal formations, one-man-one shilling debate
“Ni unafiki mkubwa kusema kuwa matatizo yetu yanatokana na idadi kubwa ya majimbo,maeneo bunge ama wadi kote nchini, tunachohitaji kufanya ni kupunguza ufisadi ambao unachangia kupotea pesa za maendeleo,”akasema Osoro.
Mbunge wa Bomachoge Chache Alpha Miruka alisema kuwa wakenya wanahitaji maeneo bunge na Mawadi zaidi na vyeo vinavyostahili kupunguzwa ni vya Maseneta Maalum, Wabunge Maalum na Wawakilishi Wadi Maalum. “Hatuwezi kukubali njia zilizopitwa na wakati ambazo zinatumika ili kuondoa matatizo ya siku za baadaye, tunahitaji pesa zaidi katika majimbo yetu, maeneo bunge yetu na wadi zetu na pia kubuni nafasi zaidi za kazi ili kuondoa
umaskini,” akasema Miruka. Mbunge wa Kuria Magharibi Mathias Robi alisema kuwa jamii ya Wakuria iliumia sana wakati ilipokuwa katika eneo la Nyanza Kusini ambapo ingewachukua siku kadhaa kupata huduma katika makao makuu ya wilaya mjini Homa Bay. “ Jamii ya Wakuria inapigania kupata jimbo lao wenyewe kwa maana iko miongoni mwa jamii tatu ambazo zinajumuisha pia Wateso na Wakuria ambazo hazina majimbo yao ili kuleta maendeleo karibu na wananchi kama maeneo mengine,” akasema Robi.