Kwa majuma kadha tumekuwa tukitoa maelezo kuhusu ubora wa maziwa ya mama kwa mtoto mchanga. Katika makala hayo tulisimulia jinsi maziwa hayo yanavyompa kila aina ya manufaa mtoto mchanga, kuanzia kinga ya mwili kuimarika kwake kiumbo na siha kwa jumla na hata uwezo wa kuona vyema hutokana na maziwa ya mama. Pia tumeelezea manufaa anayopata mama kwa kumnyonyesha mwanawe na tukasema kuamwisha huko humfaidi mama kiafya na manufaa mengine mengi ambayo mama mnyonyeshaji hupata.
Ingawa kuna mengi mengine ambayo hatujayasimulia, wiki hii tunatamatisha makala haya ya maziwa ya mama, ili kutoa nafasi kwa akina mama wajifanyie utafiti zaidi wao wenyewe, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanajielimisha juu ya mambo mengi. Kama walivyosema watangulizi wetu, elimu haiishii darasani bali inapatikana mahali popote, na kwa sababu ya vifaa vya kisasa vya mawasiliano na mitandao, mwanadamu anaweza kupata elimu kwa njia mbali mbali, bora awe na nia ya kutafuta elimu.
Katika makala yaliyotangulia, tulimalizia kwa kuzungumzia aina ya vyakula maboga ambayo huusababisha mwili kutengeneza chembe chembe nyekundu za damu. Leo tunazungumzia chakula cha nafaka ambacho kinamfaa mama anayenyonyesha hasa kinapotumiwa kama kifungua kinywa. Kifungua kinywa hiki ni cha nafaka. Wataalamu wanasema baada ya kukosa usingizi usiku kucha, akina mama wanaonyonyesha wanapaswa kupata kifungua kinywa chenye nguvu na wanasema chakula cha nafaka ni bora mno.
Nafaka baridi ina wingi wa vitamin na lishe tele kukusaidia wewe mama kupata nguvu unazohitaji kwa ajili ya kumshughulikia mwanao. Pia mchanganyiko wa matunda na maziwa ni chakula kizuri kwa mama anayenyonyesha. Mshauri mtaalamu wako wa lishe atakuelekeza aina ya matunda na jinsi ya kuyatengeza kuwa chakula bora kwako na kwa mtoto wako. Akinamama wanaonyonyesha kadhalika wanakabiliwa na upungufu wa maji katika miili yao, kwa hivyo wanahitajika kunywa maji kwa wingi. Ili kuhakikisha kwamba mwili wako una nguvu na uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha kwa mtoto wako, kunywa maji ya kutosha.
Unaweza kuchagua kunywa maji katika vipindi fulani kisha kuacha kunwa maji matupu na kunwa maji ya matunda na maziwa. Lakini uwe mwangalifu kuhusiana na kunywa vinywaji vyenye kahawa au chai. Usinwe zaidi ya vikombe vitatu vya chai au kahawa kwa siku. Katika makala ya awali tulizungumzia umuhimu wa kula matunda ya aina ya malimua. Kwa mujibu wa habari za utafiti vinywaji vinavyotengenezwa kutokana na matunda haya humsaidia sana mama mnyonyeshaji.
READ MORE
AU, UN agencies call for building resilient industries to advance Africa's development
Why is Indian tycoon Gautam Adani facing US bribery charges?
Maji hayo ya matunda ni dawa ya kuyeyusha vijiwe vinavyojiunda ndani ya figo, kwa hivyo unapotumia maji hayo, utapata manufaa ya kuepuka vijiwe hivyo ambavyo husababisha uchungu mwingi kwa figo. Vijiwe hivyo hujiunda wakati mkojo unapokuwa na wingi wa madini yanayoweza kuunda vijiwe hivyo, kutokana na kugandamana kwa mkojo.
Moja ya vijiwe hivyo husababishwa na uchache wa asidi inayopatikana kwenye matunda ya limau katika mkojo. Matunda mengi ya jamii ya malimau na maboga yana uwezo mkubwa wa kuongeza kima cha asidi hiyo kwenye mkojo wako, hivyo basi kukupunguzia uwezekano wa kufanya vijiwe vya figo Kunywa maji ya matunda haya ya jamii ya limau na kuyala matunda haya, huuwezesha mwili wako kupata mchanganyiko wa madini ya potassium na asidi ya matunda ya jamii ya malimau.
Kulingana na utafiti uliofanywa nchini Amerika, katika kipindi cha miaka arobaini iliyopita, vijiwe hivyo vya figo vilipatikana kwa wingi miongoni mwa watu ambapo hawali au kunywa maji ya matunda haya ya jamii ya limau. Kwa mujibu wa habari za utafiti, matunda haya yanapotumiwa mara kwa mara zaidi husaidia kuzuia magonjwa ya saratani au kukabiliana na magonjwa hayo.
Harakati nyingi za utafiti kutoka kwa wataalamu mbali mbali zimedhihirisha kwamba matunda haya yana uwezo wa kupunguza maambukizi na madhara ya baadhi ya saratani. Katika moja ya chunguzi, iligunduliwa kwamba watu wanaokula tunda la mzabibu au wanaokunywa maji ya tunda hili kila siku, walikwepa hatari ya kuambukizwa saratani ya mapafu.