Mzee Jaramogi Oginga Odinga

Wakati jamii ya Waluo walipohamia nchini Kenya kutoka maeneo ya Uganda na Sudan, walijitafutia makao yao karibu ziwa la Victoria mnamo karne ya 15 wakiongozwa na Mzee mmoja kwa jina la Ramogi Ajwang ambaye alichukuliwa kama miongoni mwa mashujaa wa mwanzo.

Vizaliwa waliozaliwa hatimaye walikuwa na hamu ya kufi kia kiwango chake cha umaarufu. Barubaru walimuenzi na kutamani kuwa mfano wake. Kulingana na wana historia, wanasema hiki ndicho chanzo cha mahiri wa siasa ya Nyanza, akiwemo Oginga Odinga kuwa sababu yakujibatiza jina la “Ja-Ramogi” ikimaanisha “Ni ukoo wa...” (Jaramogi Oginga Odinga) na kweli Mzee aliambulia kuwa wa ajabu, kuogopesha, kuheshimika na kinga ya jamii nzima ya Nyanza.

Wengi wanasema leo hii huwezi kusikia kilio cha ardhi kwamba kanda ya Nyanza imenyakuliwa ama kuporwa na wanyakuzi isipokuwa mizozo ya kawaida baina ya jamii kwa jamii. Yaaminika Jaramogi Oginga alifaulu kuhakikisha kwamba amelinda haki ya jamii katika kuhifadhi mashamba yao na kuwa ni bora kufa maskini lakini uzikwe kwenye ardhi yako.

Kwa miaka mingi sasa, hakujakuwa na mivutano ama maangaiko kwamba marehemu fulani ameregeshwa chumba cha kuhifadhi maiti kwa sababu ya ugomvi wa kunyimwa sehemu ya kuzikwa. Daima ameacha wasia kwamba nyumbani ni nyumbani, kuwe mashariki au magharib, kwenu ni bora.

“Maadili ya jamii yetu ni kuhakikisha kwamba mabaki ya mili yetu tunapopatwa na mauti popote pale, lazima tusafirishwe kuzikwa kwetu na tadi na mila za kitamaduni kutimizwa,” asema Ouma Oloo mfanya biashara wa uchukuzi wa tuk tuk.

Msimamo wa Jaramogi

Licha ya Jaramogi kufikiriwa vibaya na maadui wake wa kitaifa kama kiongozi wa siasa ya mkono wa kushoto (mkomunisti), muasi, mkabila, mchochezi na jambazi, yeye alibakia na msimamo wa matarajio yake ya kuwa kinara wa kitaifa.

Wengi waliowahi kuwa karibu naye, wanasema kuwa mbali na uwezo na utajiri aliokuwa nao kamwe hakuonyesha mtu yeyote yule madharau ya kimaisha. Mapenzi yake ya kitaifa na Nyanza, yalionekana mapema hususan katikati mwa mwaka wa 1940 wakati Jaramogi aliunda kampuni ama shirika la biashara kwa jina Bondo Thrift & Trading Corporation.

Hatimaye aligeuza majina kadha wa kadha ya kampuni hii kabla ya kubadilisha mwaka wa 1947 kuitwa Luo Thrift & Trading Corporation (LUTATCO). Jaramogi alinakiliwa wakati huo akisema kwamba aliamua kubadilisha jina hadi kujumuisha jamii nzima ya Waluo (Luo Thrift) ili wote wajihisi kuwa yao na kujivunia nayo.

Hali kadhalika, itakumbukwa kwamba hatimaye aliunda chama cha Kenya People Union (KPU) kwa niaba ya Wakenya waliohatarisha maisha yao kwa sababu ya uhuru wa taifa hili lakini wakapunjwa baadaye.

Mzee Jaramogi, twakumbuka shabaha yake ya kuanzisha chama cha KPU, ilikuwa ni kuwapa fursa Wakenya waliopigania uhuru wa nchi hii ambao walipuuzwa na wenzao haswa mfano mzuri ukiwa ule wa Mau Mau dhidi ya wale waliokuwa askari kanga wa wazungu (home guards).

Nguvu za Jaramogi

Kuna sababu ambazo zamdhihirishia Mzee Jaramogi kuwa kwa kweli hakuwa mtu wa kawaida. Hii inatokana na ushuhuda uliojitokeza baada ya kutofautiana baina yake na wafuasi wa aliyekuwa chipukizi wa siasa wa jamii hii miaka ya mwishoni mwa miaka ya 1950s na 1960s, Tom Mboya.

Wakati mwanasiasa Ndolo Ayah alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere mwaka 1961 akiwa pamoja na Pamela Odede, mtoto wa aliyekuwa mpiganiaji uhuru na mwanachama wa Legco (Legislative Council), Walter Odede.

Wakati huo, Tom Mboja alialikwa chuoni kutoa hotuba na kumvutia Pamela ambaye alishawishiwa kuhama Makerere ili ajiunge na mradi wa masomo ya juu Ulaya yaliyokuwa chini ya mpango wa Mboya maarufu kama 1961 Airlift.

Pamela alikuwa miongoni mwa kundi la mwanzo lililojumuisha Wangari Muta Mathai, Ojwang K’Ombudo, Muthoni Muthiga, Beth Mugo na Nicholas Mugo. Ni kupitia mpango huu wa Tom Mboya wa 1961 airlift ambapo alipata mtego wa Mboya kumwoa Pamela Odede ilhali naye Nicholas Mugo akapata fursa ya kumkamata na kufunga ndoa na Beth Mugo.

Mazingaombwe

Mzee Jaramogi alikuwa mtu wa kiajabu. Maumbile yake wengi hawakujua kwamba yanatofautiana kabisa. Watu isipokuwa wale wa karibu naye ndio waligundua kwamba alikuwa na mkono mmoja mrefu na mwingine ukiwa mfupi.

Mkono wake wa kushoto ulikuwa mfupi ukiulinganisha na ule wake wa kulia. Kulingana na ripoti ya utafiti wa maisha yake iliyotayarishwa na wasomi Daudi Kahura na Bethuel Oduo, inamnakili Thomas Odoyo akisema. “Laana la Mzee Jaramogi lilibebwa na mkono wake wa kushoto akisisitiza kuwa kweli mkono wake huu ulikuwa mfupi kuliko wake wa kulia na alikuwa na nguvu za kiajabu kuwalaani wote wanaoenda kinyume naye kisiasa ya dholuo”.

Kwa wale waliompinga Jaramogi kama Tom Mboya na wengine, walipata kujua laana lake lalemea vipi. Mfano mzuri ni ule unaokumbukwa wa Nyamolo Okal (wengi wa jamii hii ama wanahistoria wanajua kisa hiki) ambapo alimkasirisha Mzee Jaramogi katika mkutano wa hadhara wa Pat-Onditi hadi kuwajibika Mzee amuonyeshe kuwa ni moto wa kuotea mbali.

Siku hiyo, Jaramogi kwa hasira, alimwelekeza Nyamolo Okal kidole cha shahada cha mkono wa kushoto na kumuonya kwa lugha: “Nyamolo Okal in ema iketho bucha kamae, wanane ka nine od bura?” akimaanisha kwa tafsiri kuwa “Nyamolo Okal, wewe ni mmoja wa wale wanaoniharibia mikutano yangu, tutaona kama wewe utauona mlango wa bunge maishani mwako”.

Na kweli baada ya kisa hiki, Nyamolo ni kana kwamba alilaaniwa. Maisha yalimwendea kombo kwa kumpinga ama kukejeli Mzee Jaramogi licha ya kuwa Nyamolo Okal alikuwa Mkenya wa kwanza kusimamia shule ya upili ya Kakamega High baada ya kumaliza chuo cha Makerere.

Mlango wa bunge pia aliuona akipita nje ya majengo yake hata baada ya kuwania ubunge wa Nyakach miaka ya 1966, 1969 na 1974. Baada ya rafiki yake Tom Mboya kuawa 1969, maisha ya Nyamolo yalizidi kudidimia na biashara kufifia. Nyamolo alifariki maskini wa kuhuzunisha.