Rais Uhuru Kenyatta.

Wakati wabunge wa Mombasa walipokuwa wakijipiga kifua muda mfupi baada ya mkondo wa kwanza wa marekebisho ya sheria inayoruhusu biashara za meli na uchukuzi ya Merchant Shipping Act 2019 kupingwa na wabunge, hawakujua kwamba nguzo ya nchi ni Rais ambaye anapaswa kuingilia mahali ambapo walafi wameenda kombo kisheria.

Hata kabla ya kuidhinishwa rasmi na rais kuwa sheria, wabunge wa pwani wakiongozwa na kijana wao wa mkono katibu mkuu wa chama cha makuli nchini cha Dock Workers Union, Simon Sang, tayari walikuwa wanatafuta ukumbi wa kuandaa sherehe za kufaulu kufi lisi ndoto ya vijana 1000 ambao walikuwa wanasubiri kuajiriwa zaidi na kampuni ya meli ya MSC. Sang ambaye amekuwa dalali mkubwa katika kuwakutanisha baadhi ya wabunge na matajiri fulani wanaomezea mate kiegezo kinachong’ang’aniwa bandarini cha CT2, alikuwa mstari wa mbele kusaka sehemu ambayo ingewaleta viongozi wote kusherehekea ushindi wao.

Habari za ndani zaidi zawalenga wanasiasa fulani wa kitaifa ambao walikuwa wako tayari kudhamini sherehe hizi. Mnamo Juni 19 mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta aliuregesha tena mswada huu bungeni na kumwamuru Spika wa bunge la kitaifa nchini Justin Muturi kuwapa fursa wabunge tena kuupiga msasa akisema kwamba jinsi mapendekezo yalivyoshinikizwa na wabunge kamwe hayana msingi wa kuyajali maslahi ya vijana wenyeji wa mazingira ya bahari na fursa ya ajira na uchumi ambao serikali imeweka kipao mbele.

“Ikiwa sheria hii itaachiliwa vile ilivyo kwa mapenzi ya wabunge kamwe haitowasaidia vijana chungu nzima wa pwani na nchi nzima ambao wamepangiwa kufaidi kupitia shirika hili la kitaifa la KNSL ambalo limo miguuni mwa bandari ya Kenya, KPA”, warakha wa Uhuru kwa Muturi unanukuu.

Naye spika Muturi anasisitiza maelezo ya Rais kwamba hatimaye anapendekeza kifungu tasa cha Merchant Shipping Act 16 (1A) kinachonuia kuwaregesha vijana zaidi ya 200 ambao wameajiriwa kupitia kwa KNSL na kampuni shiriki ya MSC toka mwaka jana kifutiliwe mbali.

Hiki kifungu kinapinga kiegezo cha CT2 (Container Terminal 2) kutoruhusu kampuni yoyote kuruhusiwa kuhudumu biashara za meli (kupakua na kupakia) na shughuli nyinginezo za baharini ikiwa haina haki miliki asilimia 100% za kitaifa (umma).

Kulingana na sababu ambazo Rais anajitetea kutupilia mbali mapendekezo gaidi ya wabunge waliyopitisha mnamo Jumatano ya Juni 12, 2019, anazungumzia kuwa ni ukosefu wa utu kupinga huduma za shirika la kitaifa la KNSL lenye umiliki wa hisa zaidi chini ya usimamizi wa KPA kwa sababu za kisiasa za matumbo ya wanasiasa wanaojitafutia mwanya kibiashara wala siyo kwa sababu ya wananchi wao.

Hatua ya wabunge kuimba usiku na mchana kupinga huduma za KNSL bandarini limezua kumbukumbu kwa umma jinsi viongozi wanavyowasulubisha wananchi wao kwa kiwango kidogo cha pesa. Taarifa za ndani zaelezea kuwa kampuni na matajiri ambao wameamua “kumwaga mboga, wakimwagiwa ugali”, walichanga mamilioni ya pesa kuwasambazia wabunge kama vile walivyopokea hongo za elfu 10,000 kila mbunge wakiwa ndani ya vyoo walipoangusha mswada wa ripoti ya “sukari”.

Sherehe fupi

Muda mfupi baada ya kikao cha bunge kumalizika na mswada wa kuzima huduma za KNSL na MSC kampuni ambayo imeanza kuajiri vijana tele, wabunge Abdulswamad Nassir (Mvita), Ali Mbogo (Kisauni) na seneta wa Mombasa Mohamed Faki walitoa taarifa zao mitandaoni ya Facebook kujipiga kifua kwamba wamefaulu kutimiza kazi yao.

Wabunge wengine wa pwani pia walijumuika nao wakifurahia kwamba ushindi huu ni dhahiri wale wote ambao wameajiriwa na kampuni ya MSC wanaohudumu kwenye meli zao kote ulimwenguni watarudi kuteseka tena na familia zao nyumbani mradi wao kama viongozi, mifuko yao imejaa pesa za milungula kutoka kwa matajiri waliowasukuma kupinga hadi dakika ya mwisho wa mswada huu.

Seneta wa Kwale Issa Boy Juma, mbunge wa Rabai William Kamoti, mbunge wa Kaloleni Paul Katana, mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, mbunge wa Lungalunga Khatib Mwashetani, mbunge wa Kinango Benjamin Tayari, mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya miongoni mwa wengine ambao walikuwa wakichungulia yote yanayoendelea bungeni lakini wamekwisha kukamata hela pia walikuwemo.

Machozi ya damu

Huku viongozi wa pwani wakisherehekea kuangushwa kwa mswada wa kuwaokoa jamii kutoka kwa pato kuu la bahari, wazazi wa vijana 16 na wale 42 waliochukuliwa mwezi uliopita na kampuni ya MSC kama makubaliano muafuaka na serikali ya kutoa ajira melini, walikuwa wanabubujikwa na machozi ya damu. Wengi wa wazazi wamekuwa wakiwalaani viongozi wao ambao badala ya kufuatilia vyema suala hili ambalo limeanza kutoa nafasi za ajira kwa vijana, ni hao wanaopinga kazi hizi ilhali hakuna hata mbunge mmoja ambaye amewahi kubuni nafasi yoyote ya kazi.

Habari za ujasusi zinatoboa kwamba hatua ya rais Uhuru kuregesha mswada huu bungeni, kumewapunguza presha wazazi ambao walikuwa wamepanga kuandamana moja kwa moja hadi kwa afi si za wabunge wa kuanzia kaunti za Kilifi , Mombasa na Kwale kuwauliza ni wapi vijana wao walioajiriwa watakuwa endapo mkataba wa KNSL na MSC utakatizwa kwa sababu yao.

“Hatuwezi kukubali tabia za wabunge wetu kupinga kila kitu ambacho hawajahusishwa kibiashara kudhuru maisha ya watoto wetu ambao wameanza kusaidia familia zao. Niko na watoto wanne ambao nimewafundisha kwa pesa zangu mwenyewe na sasa wako ulaya melini sasa wabunge wanataka niwapeleke wapi wakiregeshwa,? Anajiuliza mzazi wa Margret Zawadi ambaye anahudumu meli ya Meriviglia.

Wengine ni Tanisha Abdul, David Randu wanahudumu meli ya MSC Lirica, Robert Lewa na Maureen Nkatha, Mary Mueni akiwa na meli ya MSC Musica, Raphael Bakari akiwa na MSC Splendida, John Mwarabu, Stephen Gari na Mohammed Bechari wakiwa meli ya Lirica, Rudguillet Otieno, Ali Mohammed wakiwa MSC Meravigila, Eng. Luke Samba (afi sa wa KMA), nahodha wa pekee wa kike wa meli ya kifahari Elizabeth Marami miongoni mwa wengi walio majuu.

Udadisi wa ndani Shinikizo la kutupilia mbali sheria hii ilitokana na msukumo wa matajiri na kampuni ambazo zilikosa kandarasi ambayo shirika la kitaifa linalonuiwa kutoa huduma za meli na biashara za baharini la Kenya National Shipping Line (KNSL) kufaulu kushikamana pamoja na kampuni ya kimataifa ya MSC yenye huduma ziada za meli za abiria (utalii) maarufu kama Cruise Ships.

Kampuni ambazo zimehusika kusaka zabuni ambayo KNSL na MSC zimepata kuhudumu huduma za meli na biashara kwa niaba ya Kenya chini ya usimamizi wa halmashauri ya bandari nchini, KPA, zaaminika zimekuwa katika mstari wa mbele kudhamini msukumo huu kwa kuwatumia wabunge wa pwani wakiongozwa na wasuki wa jamvi zima hili Abdulswamad Nassir (Mvita), Ali Menza Mbogo (Kisauni) na seneta wa kaunti ya Mombasa, Mohamed Faki. Ni kampuni hizi ambazo zinasemekana kuwatumia wabunge na kupigania nafasi ya CT2 kisiasa kwa kuhakikisha pesa zimetembea ndani ya bunge na mifuko ya wabunge kama zilivyotembea zile za ripoti ya sukari kuhakikisha wamefaulu.

Ingawa hivyo sasa itawabidi kupiga kura ya ushindi wa wabunge zaidi ya 235 bungeni kupinga mswada huu utakapofanyiwa ukarabati kama mapendekezo ya rais.

Msimamo wa serikali ya kaunti ya Mombasa

Gavana wa Mombasa Hassan Joho hajatia guu lake ndani ya patashika hili ijapo ameelezea kinaga ubaga kwamba kutoka mwanzo, ilikuwa ni vyema kwa kamati kuu ya uchumi wa bahari (Blue Economy) kujadiliana vyema na viongozi wa mashinani kutafakari faida za pande zote mbili.

Kulingana na jinsi ya mambo yalivyo, kunao uwezekano mkubwa sasa wa serikali ya kaunti kushirikiana zaidi katika mikakati zaidi ya kufafanua suala hili kwa kuweka vichwa pamoja na uwakilishi wa kamati ya uchumi wa bahari na halmashauri kuu ya bandari nchini KPA, kujadili ufanisi wa kuboresha marekebisho ya mswada huu kuambatana na manufaa ya kila mhusika kama alivyopendekeza rais.

Naibu wa gavana wa Mombasa Daktari William Kingi ananukuliwa akiunga mkono msimamo wa gavana kwamba kuregeshwa kwa mswada huo bungeni kwa ukarabati mahsusi ni jambo la kutia moyo kwa washika dau wote.

Inasemekana kwamba hatua hii itawezesha serikali ya kaunti chini ya uongozi wa Gavana Joho kujadili vyema na kuhusisha kila upande kuona kwamba hakuna vizuizi vya kuzuia kila sekta kuvuna faida za uchumi wa bahari ambapo kitovu chake ni kaunti ya Mombasa.

Miongoni mwa faida ambazo vijana wanapigania ni pamoja na mafunzo ya kisasa ya ubaharia na kazi nyingine za baharini vile vile uchumi na biashara. Ufanisi huu umeanza kujitokeza kupitia kwa chuo cha Bandari ambacho awali kilisimamiwa na halmashauri ya bandari nchini kilichogeuzwa kuanza kutoa mafunzo maalum ya uchumi wa bahari na kuitwa Bandari Maritime Academy.

Kazi zitapatikana siyo tu humu nchini bali hata za kimataifa.

Hali kadhalika kulingana na utafi ti kunalo hakikisho kamili kwamba kuna kazi zaidi ya 2000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano. Jambo lingine ambalo linawapa maisha vijana wanaochipukia kazi, ni kuwa bandari ya Mombasa itakuwa kiegezo cha kusafi risha makasha ama mizigo kwa bandari nyingine kama kitovu cha usafi ri wa baharini.