[Picha: Standard]

Wakaazi katika eneo la Takaungu kaunti ya Kilifi wanaendelea kutofautiana kuhusina na ujenzi wa kituo cha kuhifadhi gesi, kwa madai kuwa kujengwa kwa kitua hicho kutasababisha uharibifu wa mazingira.

Baadhi ya wakazi hao wanasema hawataruhusu kituo hicho kujengwa eneo hilo wakidai kuwa sekta ya uvuvi ambayo ndiyo tegemeo kubwa kwa wakazi eneo hilo itasambaratika kutokana na kutupwa kwa takataka kuingia baharini.

Waekezaji wa kibinafsi wamepanga kujenga kituo cha uhifadhi gesi katika eneo hilo.

Wiki iliyopita viongozi katika eneo hilo walikosa kuhudhuria kikao baada ya chifu wa eneo hilo na kamishina wa kaunti ya Kilifi kususia kikao na wakaazi hao.

Wakazi hao wamewalaumu viongozi hao kwa kutohudhuria mkutano huo wakihofu kwamba mwekezaji huyo atachukua nafasi hiyo ya mgawanyiko  wa wakazi kuendeleza mradi huo.

Kasumba Mbango amabye ni mzee wa mtaa ene hilo amesema mradi huo ulikuwa umesimamishwa kutokana na kuwa huenda ukasababisha uharibifu wa mazingira.

“Makubaliano yaliafikiwa mwaka uliopita kwenye mkutano ambao uliandaliwa na mamlaka ya usimamizi wa mazingir  NEM , sisi tayari tunaathirika na ugonjwa wa kifua kikuu na matatizo ya macho kwa sababu ya vumbi la simiti. Hatutakubali shida zaidi zitukabili,”akasema Mbango.

Ripoti ya athari ya mazingira kwa mradi huo ambayo iliwasilishwa kwa NEMA ilionyesha kuwa kujengwa kwa  hifadhi hiyo kutasababisha uchafuzi wa mazingira  ndani ya bahari pamoja na kuathiri maisha ya wanadamu.

Hata hivyo wakazi hao wanasema gasi hiyo itamwagika na kuingia baharini ambapo itaathiri maisha ya samaki baharini na kuharibu uchumi wa watu wa  Takaungu.

“Watu wengi eneo hili hutegemea uvuvi wa samaki ambayo ndiyo kazi yao ya kila siku, nao wake zetu hupata kipato wakati wanapouza samaki, sasa tutafanya nini endapo samaki wataangamia kwa sababu ya gesi ambayo itamwagika ndani ya bahari? ,”akauliza Katana Chengo.

Mkutano huo wa wiki iliyopita ulikuwa unapania kuleta pamoja maoni ya wakazi wanaoishi eneo hilo, ili kutafuta njia mwafaka ya kutatua mzozo wa kujengwa kwa hifadhi hiyo.

Mwekezaji ambaye ni Taifa Gas Kenya amesema wahusika wa pande zote mbili wamechelewesha mikutano ya wakazi ya kutoa maoni yao kuhusiana na ujeni wa hifadhi hiyo ya gasi.

 “Tunaonelea kabla ya kuanzisha kazi hii tunawataka washikadau wote eneo hilo kuwapatia nafasi wakazi kutoa maoni yao, na kutatuliwa kwa shida hizi za kutoelewana,” akasema mkurugenzi wa kampuni hiyo Victor Onyango.

Onyango amesema ekari 2.29 ya ardhi ndiyo itakayotumika katika eneo hilo akitaja kuwa kampuni hiyo imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa itathibiti uchafuzi wa mazingira eneo hilo.  

Hata hivyo wale ambao wanaunga mkono kujengwa kwa hifadi hiyo wanasema  wanataka kazi hasa wakisema kuwa wamekuwa wakiishi bila ajira na fursa hii ni nafasi kwao kupata ajira kutokana na ujenzio huo.

Wanasema hata ujenzi wa mtambo wa simiti ya Mombasa Ceement ulikataliwa na wakazi lakini mara ya mwisho ukakubaliwa na kujengwa.

“Ni mara nyingi tumeathirika na viwanda kwa hivyo sisi tunakubali kijengwa ili tupae kazi hapa vijana wengi hawana kazi ,” akasema Suleiman Salim.

Mwezi Octoba 15 mwaka jana familia zaidi ya 200 ziliwasilisha mkataba wa makubaliano  kwa gavana wa Kilifi Amason Kingi pamoja na tume ya ardhi nchini na kuiandikia barua mamlaka ya mazingira nchini NEMA mwezi Novemba 15 kutaka idara hizo kutotoa liseni  kwa Taifa Gas Kenya ya kuanzisha mradi huo.

"Kupitia malalamishi ambayo yalitolewa na wakazi, tume ya ardhi sasa imetoa mwelekeo kutotoa liseni hadi pale makubaliano yatakapoafikiwa, NLC itafuatilia utekelezwaji wa maelekezo haya kwa mujibu wa mamlaka yake ," aliandika mwenyekiti wakati huo Mohammed Swazuri.

Barua hiyo pia iliwasilishwa kwa idara ya ujenni na mipango kaunti ya Kilifi ,afisi ya katibu katika wizari ya Mazingira nchini, pamoja na afisi ya mkurugenzi katikia tume ya kuthibithi Kawi nchini.