Wanawake wengi nchini Kenya bado wameachwa nyuma katika umiliki wa simu za mikononi na matumizi ya mtandao kupitia simu hizo ikilinganishwa na wenzao wanaume.

Kwa mfano japo pengo la umiliki wa simu za rununu ni asilimia sita baina ya wanawake na wanaume hapa nchini, hata hivyo tofauti ni kubwa zaidi kwenye matumizi ya mtandao kupitia simu hizo kwa asilimia 26 pekee ya wanawake ikilinganishwa na asilimia 43 ya wanaume.

Haya ni kwa mujibu wa utafiti mpya uliozinduliwa majuzi unaoangazia suala zima la pengo jinsia lililopo ulimwenguni katika umiliki wa simu za rununu na matumizi ya mtandao kupitia simu hizo.

Ni utafiti ulotekelezwa na shirika la GSMA katika nchi 18 ulimwenguni zenye mapato ya chini na wastani. Kwa ujumla matokeo ya utafiti huo yanaashiria kwamba hasa wanawake wengi mno katika nchi hizo bado wapo nyuma kuambatana na suala hili.

Hadi wanawake milioni 197 kwa ujumla wanakisiwa kutomiliki simu za rununu ikilinganishwa na idadi ya wanaume wenye simu. Hii ina maana kwamba kuna uwezekano wa hadi asilimia 10 ya wanawake kutomiliki simu hizo ikilinganishwa na wenzao wanaume.

Vile vile pia, wanawake takriban milioni 313 hawatumii simu za mikononi kuingia kwenye mtandao na hii inawakilisha pengo la kijinsia la asilimia 23 katika matumizi ya mtandao kwa kigezo hicho.

Changamoto kuu inayowakwaza wanawake wengi kutomiliki simu za mikononi katika nchi zote 18 zilizojumuisha utafiti huo ni uwezo wa kifedha, ripoti hiyo inaeleza.

Na hususan Kenya, sababu nyingine zilizo orodheshwa ni kama changamoto za kielimu, sababu za kiusalama zinazoambatana na kumiliki simu pamoja na wanawake wengi kutoona thamani ya kuwa na simu katika maisha yao.

Kwa upande mwengine, hata baina ya wanawake wanaomiliki simu za rununu imesemekana kwamba sababu zinazowazuia wengi wao kushindwa kutumia mtandao ni kama zile zinazowakwaza kumiliki simu hizo. Kwa mfano simu zenye uwezo wa kuingia mtandaoni ziko ghali ikilinganishwa na zile nyingine.

Vile vile changamoto za kielimu na ujuzi dijitali, wanawake wengi kutoona umuhimu wowote wa kutumia mtandao pamoja na hofu za usalama kutokana na mitindo potofu ya mitandaoni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo hapa nchini kwa mfano, kati ya wanawake ambao wanafahamu kuwepo kwa uwezo wa kuingia mtandaoni kupitia simu za rununu hadi asilimia 46 walitaja suala la gharama kama kikwazo kwao.

Asilimia 24 walitaja changamoto za kielimu, asilimia 14 waliripoti kwamba hawakuona umuhimu wowote wa kutumia mtandao na asilimia nane wakaeleza suala la kuhofia usalama wao.  

Ripoti yaeleza kwamba upunguzaji wa pengo lililopo baina ya wanawake na wanaume ulimwenguni utakuwa na faida kubwa za kiuchumi hasa katika upanuzi wa mapato ya kitaifa (GDP).

“Shirika la GSMA linakadiria kwamba pengo jinsia hili kubwa kwenye matumizi ya mtandao kupitia simu za rununu likipunguzwa, kuna uwezekano wa kuongeza pato la taifa kwa dola bilioni 700 kwenye nchi hizi kwa miaka mitano ijayo,” inasema ripoti hiyo.