Kikundi kimoja cha akina mama walemavu kaunti ya Mombasa wanatengeza sodo au pedi zinazo weza kutumiwa tena na tena hadi kipindi cha takriban miaka miwili.
Pedi hutumiwa siku za hedhi na wanawake ili kuhakikisha unadhifu katika masiku hayo pamoja na kuwawezesha kuendeleza shughuli zao za kawaida kwa ustaarabu.
Hata hivyo wasichana wengi wanaotokea familia zisizojiweza hukumbwa na changamoto kwa sababu ya gharama ya kununua pedi za kawaida zinazo uzwa madukani. Na hususan kwa wasichana hali hii ambao pia ni wanafunzi tatizo hilo huathiri masomo yao kwa kushindwa kwenda shuleni siku zao zinapowadia.
Hili ndilo zingatio kuu lililowasukuma akina mama hao walemavu wa Tunaweza CBO iliyo maeneo ya Bombolulu, na kutathmini ni kipi wangeweza kufanya kuwaokoa wanafunzi wa kike wanaotoka familia masikini.
READ MORE
KRA in fresh plan to weed out graft at port
Junior golfers set for battle at Nyali course
COP29: Investment in Solar-powered pediatric theatres will ensure patient safety
Na baada ya kusumbua vichwa kwa muda mrefu, safari ambayo ilikua na pata potea hatimaye waliweza kubuni sodo muafaka walizotengeneza kwa mikono yao yenyewe.
“Kabla tufanikiwe kupata matirioli aina ya Flannel tunayoitumia hivi sasa, tulijaribu kutumia hata blanketi hapo mwanzo lakini tukaona ilikuwa haiwezi kunyonya majimaji vizuri na kudhibiti utiririkaji,” alieleza Charity Chahaso, mwenyekiti wa kikundi hicho.
Na kwa kutumia ujuzi walionao katika usanii wa ushonaji nguo, waliweza kubuni pedi hizo ambazo wanatengeza kwa kutumia mchanganyiko wa mabaki ya vitambara vya vitenge na hiyo aina ya matirioli inayojulikana kama Flannel.
“Na pia kwa kuzingatia vile hizo pedi za kawaida zinachangia uchafu wa mazingira kwa kutupwa ovyo tukaona tunaweza kutengeza kitu ambacho kitawasaidia wasichana wetu pamoja na kupunguza takataka,” alisema Charity.
Kuanzia 2016 walipoanza kutengeneza pedi hizo hadi sasa wameshafaulu kupeana sodo hizo kwa takriban wasichana 1000 hususan kwenye shule zilizoko mitaa ya mabandani kaunti ya Mombasa.
Upekee wa sodo za akina mama hao ni kwamba wao hutengeza taulo nane za pedi pamoja na makasha mawili yakuvishwa taulo hizo, halafu hizi zote huwekwa kwenye pakiti moja. Pakiti hiyo moja ndio anayopewa msichana na ambayo ataweza kuitumia kwa kipindi hadi cha miaka miwili.
“Msichana akishatumia pedi moja anaiosha kama unavyoosha nguo yeyote ile na kuweza kuitumia tena. Kati ya shule tulizowapelekea pedi hizi, takriban asilimia 98 walifurahia sana ubunifu huu na hata wanapendekeza turudi tena kuwapelekea zaidi,” asema Charity.
Mazingira na kemikali zinazodhuru
Pia wanaeleza kwamba mbali na kuwa pedi za kawaida zinadhuru mazingira kwa kutupwa tupwa ovyo kila mahala na kwamba zinapotupwa zinachukua muda mrefu sana kuoza, athari nyingine ni kwa watumiaji wenyewe. Wanadai kwamba baadhi ya viungo vya kemikali kwa sodo za kawaida huwa hazichukuani vyema na ngozi kwa watumizi wengine.
“Takriban asilimia 58 ya watumiaji wa sodo za kawaida huwa wanadhurika aidha kwa kupata maumivu au matatizo mengine ya kiafya. Lakini wakitumia pedi mbadala kama hizi hawatapata matatizo hayo,” asema Lucy Chesi, mwanachama mwengine wa kikundi hicho.
Ubunifu wa akina mama walemavu hawa umewavutia wengi. Kwa mfano, baada ya kuona matangazo kwenye mtandao wa Facebook mjerumani mmoja alitaka atengezewe pakiti 200 na kusafiri nazo Ujerumani mwaka jana.
Na hata sasa kikundi hicho kimeshirikiana na shule ya Aga Khan Academy ya Mombasa juu ya mradi huo.
“Katika huo mpango wanafunzi wa Aga Khan Academy watakuwa wanatutembelea kila mwezi ili tuwape mafunzo ya kutengeneza pedi,” alifichua Lucy.
Pedi kwa wanafunzi huwa wanapeana bure na hazilipishwi. Na Tunaweza CBO wanaeleza kwamba mradi huo hutegemea ufadhili wa watu wanaotaka kusaidia jamii kuwapatia usaidizi kwa kuwawezesha kutengeza bidhaa zenyewe.