Wahenga walisema baada ya kisa ni mkasa. Katika kijiji cha Kakoyi Kona, kaunti ndogo ya Malava kaunti ya Kakamega kalameni mmoja aliyeshukiwa kuwa mchawi, alikiona hadharani hicho kinachoitwa cha mtema kuni, baada ya kuzua ugomvi na ndugu yake kisha nduguye akaamua kumuanika hadharani akiwa uchi wa mnyama mbele ya  wanakijiji.

Wanakijiji waliojawa na ghadhabu walijitokeza kwa fujo na kufurika furi na kuingia hadi chumbani mwa kalameni huyo mwenye mke na watoto na kupata chungu kinachodaiwa ni cha uchawi.

Baadaye wanakijiji hao walifanikiwa kupata aina mbalimbali za vifaa ambavyo vinasifika kwa ushirikina, pamoja na picha za watu wanao semekana kwamba baadhi yao wameaga dunia. Miongoni mwa vitu vilivyopatikana, ni orodha ya majina ya watu ambao baadhi yao wapo hai  na wengine hawapotena.

Kalameni huyo mwenye umri wa kati, ambaye pia ni ngariba alitunukiwa bonge la makonde kwani alipewa kichapo cha nyoka kisa kilichoamuliwa na OCS pamoja na maafisa wengine wa kituo cha polisi cha Kabras.

Maafisa hao waliwasihi wanakijiji hao kwa heshma wamkamate kalameni huyo ambaye sasa yuko kwenye hospitali chini ya ulinzi mkali, kwani anatarajiwa kufikishwa mbele ya mahakama ya Butali.

Jamii ya kalameni huyo akiwemo mke na watoto walikariri kisa hicho na kudai kuwa walifahamu jambo hilo, bali walishindwa jinsi ya kusimulia kwani wangeuawa.