Moyo wangu umejawa na simanzi. Nasikitishwa sana na hali ya nchi yetu. Hali hii inazidi kuzorota. Kwenye runinga na magazeti twaelezwa kwamba uchumi uko imara. Hali halisi ni tofauti kabisa! Wenyenchi wanakosa chakula cha msingi!

Unga wa ugali sasa umegeuka kuwa kumbukumbu tu kwenye vichwa vya wengi. Kipenzi cha wengi, ugali, sasa haupatikani kwa urahisi. Eti haya yote kwa kisingizio cha ukosefu wa mahindi nchini. Hadithi ya kupotea kwa mahindi na kuagizwa kwa mahindi toka nje bado twaiwazia.

Wakulima kila mwaka wachanika kwenye mipini makondeni mwao na mazao hayo yanaishia kwenye maghala ya kitaifa. Iweje tukakosa mahindi mwaka huu? Hasa wakati ambapo tumekaribia kufanya uchaguzi? Chakula cha msingi kimegeuzwa bidhaa ya kufanya siasa?

Mipaka yetu inafuja! Nchini humu wanaingia adui usiku kucha. Familia nyingi tayari wamewapoteza wapendwa wao, raia na askari sawa. Walio na wana, ndugu au dada kwenye vikosi vya usalama wanapiga dua kwa maulana awalinde walalapo-iwapo wanapata hata lepe. Iweje hivyo? Ni lipi hasa linaendelea kule Lamu? Kaskazini mwa nchi pia hakukaliki? Sehemu za bonde la ufa kama Baringo pia imegeuka ngome ya wevi wa mifugo. Ina maana hakuna linaloweza kufanywa kusitisha haya yote? Usalama wa wananchi unahitaji kuhakikishwa na ni jukumu la serikali yoyote ile kuwalinda wananchi wake.

 

Binafsi nimechoshwa na uongozi wa kusema tu. Wengi wa wale tuwaitao viongozi ni matapeli. Wazuri kwa kutoa miadi kisha kutokomea miaka mitano kabla ya kurejea kuyatoa miadi yale yale. Hawayatekelezi waliyoahidi kamwe! Wamebobea katika uporaji wa mali ya wasonacho pamoja na kuharibu mali ya umma. Tafakari jinsi pengo lililopo kati ya wenyenacho na wasonacho laendelea kupanuka. Utengano wa aina yake!

 

Tunapoelekea kufanya uchaguzi, zingatia sana hali ilivyo kwa sasa. Shida zikija zatuathiri sote pasi kujali kabila. Hivyo basi tuwachague viongozi ambao wanajali maslahi ya kila mwananchi si waroho na wabinafsi walio mbioni kujizolea mali kutokana na jasho la walipa ushuru. Pana haja ya kubadili mfumo mzima wa uongozi hapa kwetu.

Ufisadi sasa umekua donda ndugu hapa nchini, na tusipobadili mfumo mzima, mabadiliko yoyote yale bado yataadhiriwa na ufisadi. Suala la ukabila sasa umekua wimbo kwa midomo ya wengi, hata mataifa ya nje. Ninasubiri kwa hamu, ule wakati ambapo tutafanya uamuzi wa kuwachagua viongozi bila ya kuzingatia kabila.

Hayati mwalimu Julius Kabarange Nyerere ataendelea kunukuliwa kwa kile alichosema akiwahutubia watanzania miaka ya nyuma kuwa, “Katika karne ya 21 tupande basi la ukabila? Huko ni upumbavu na ni hatari” Kauli hii ina maana kwetu hata leo. Sisi ndisi tutakaojinasua kutoka kwenye mtego wa ukabila. Tuuvunje utamaduni huu ambao kwa muda sasa umekua kigezo cha kufanya uchaguzi na hata kupata ajira.

 

Changamoto ipo kwetu sote! Tuwe na uzoefu wa kuwachuja viongozi wasiotekeleza wajibu wao sawasawa. Tusikubali kupigana vita tusivyoelewa vilikoanzia. Twahitaji amani humu mwetu hata baada ya Agosti 8.