Msongamano mkubwa wa matrela ukiendelea kushuhudiwa katika Barabara Kuu ya Eldoret-Malaba viongozi wa Magharibi ya nchi sasa wanashikiza suluhu ya haraka kuafikiwa baina ya mataifa ya Kenya na Uganda kurahisisha uchukuzi. 

Viongozi hao wamehusisha msongamano huo na kujikokota kwa shughuli za upimaji wa madereva hao kubaini iwapo wameambukizwa virusi vya korona au la.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi wamesema kuwa hali hiyo imetokana na utepetevu wa viongozi wanaohusika huku akiitaka serikali kumwajibisha Waziri wa Afya Mutahi Kagwe. Wamunyinyi aidha anapendekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuwapima madereva katika maeneo ya Mombasa, Miritini na Malaba

Kwa upande wake Mbunge wa Teso Kaskazini Oku Kaunya, ameisuta serikali ya Kenya kwa kushindwa kuwapima wananchi wake katika mpaka wa Malaba huku shughuli hiyo ikiachiwa tu taifa la Uganda.

Haya yanajiri huku madereva wa Kenya wakiendelea kutaabika kwenye foleni wengi sasa wakilazimika kuishi na makahaba ambao wamekodisha nyumba kando kando ya Barabara Kuu ya Eldoret- Malaba wakisubiri kupimwa kabla ya kuruhusiwa kuondoka. 

Baadhi ya wakazi eneo hilo wamegeuza nyumba zao kuwa vyumba vya kukodisha kuwafaa madereva hao huku wengi wakilalamikia hali ngumi ya uchumi kumudi kodi za nyumba hizo. Vilevile wameendelea kulalamikia dhuluma dhidi yao nchini Uganda na hata kuibiwa mali zao.

Msangamao huo umekuwapo kwa muda wa miezi miwili sasa tangu Uganda ianzishe shughuli za upimaji huo kabla ya kuwaruhusu kuendelea na safari zao kwenye mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki.