Aisha Jumwa.

Wakati mwanasiasa Karisa Nzai Munyika alipoanza kumvizia mbunge wa Malindi miaka ya 2000s, alijiua wazi Aisha Jumwa Karisa siyo mtu wa kuraukia. Wote walipatana wakiwa wanasisasa, bwana akiwa diwani wa Manispaa ya mji wa Mombasa na mke akiwa diwani wa Takaungu, baraza la mji wa Kilifi .

Mke akiwa diwani, alibahatika pia kuchaguliwa kama mwanamke wa kwanza kuwa mwenyekiti wa baraza la mji wa Kilifi. Bwana naye akaishia kuwa naibu wa Meya wa Mombasa kabla ya zunguluke ya maisha kuwageukia miaka ya 2013-2014.

Karisa na Jumwa walichanika baada ya kuishi pamoja kwa miaka isiyopungua tisa. Licha ya kuwa alifaulu kumjengea nyumba ya wastani sehemu ya Mtwapa pia aliweza kulipa kiasi Fulani cha mahari kwa wazazi wa mheshimiwa kuhalalisha ndoa yao.

Baada ya kutimuana mwaka 2014 muda mfupi toka Aisha kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa kina mama kaunti ya Kilifi na Nzai mwakilishi wa wadi ya Jomvu, Mombasa, bwana alikumbuka kwamba huenda akatendwa kama mwenzake alivyofanywa kwa kushindikizwa hata kwa naibu wa chifu kuregeshewa mahari yake.

Bwana wa kwanza wa Aisha Jumwa alimshindikiza unyo unyo hadi kwa afi si ya naibu wa chifu kumkabidhi upuzi wake wa mahari uliokuwa ukimkosesha usingizi wa vigombe na vimbuzi pamoja na elfu ishirini. Karisa Nzai ambaye alijaribu kuwania ubunge wa Jomvu mwaka 2017, aliamua kufunga mdomo, macho na masikio kuhusu suala la kupayukia chanzo cha kukatika kwa uhusiano wake na Aisha Jumwa.

Wote ni wanasiasa wanaotambua siasani hakuna hadui wala Rafiki.

Fungate

Kulingana na marafi ki wao wa karibu, uhusiano mzuri wa fungate ya hawa wawili ulinoga kweli kweli kwa miaka ipatayo tisa. Ilifi kia wakati ambapo mmoja wao (Aisha Jumwa) alianguka udiwani huku bwana Karisa Nzai akiendelea kama diwani uchaguzini wa 2007-2013.

Ndani ya siku zao za furaha, wapendwa hawa (nyakati hizo) walibahatika kumpata mtoto msichana ambaye ndiye kitinda mimba cha mheshimiwa Aisha na mtoto wa tatu katika uzazi wake wa Watoto watatu. Kabla, alikuwa na watoto wawili kutoka kwa ndoa yake ya mwanzo.

Kwa upande wake, Karisa Nzai alijua anapambana na hali ngumu ya kumdhibiti mwanasiasa huyu wa majeli na sauti ya mngurumo unaoweza kumtoa nyoka pangoni. Kwa kuhalalisha ndoa yao, yadaiwa kwamba Karisa Nzai alitoa mahari inayoambatana na utamaduni na mila za jamii yao ya Wagiriama.

Ijapo hatujapata usahihi wa kiasi kamili alichotoa kama mahari, inabainika gharama yote inasimamia takribani elfu tisaini licha ya mapochopocho ya mbuzi na kadhalika.

Ikiwa Aisha Jumwa lilikuwa jiko lake la pili kama mwanamume halisi wa kiafrika, Nzai alibobea kisiasa kati ya 2007 hadi 2013 akiwa naibu wa Meya wa jiji la Mombasa, mdogo wa John Mcharo aliyekuwa Meya.

Nyumba Mtwapa

Ni wakati huu ambapo alichukua jukumu lingine la kupalilia mizizi ya penzi lake kwa Aisha Jumwa kwa kumjengea nyumba ya wastani katika maeneo ya Mtwapa kama hakikisho la kuona kwamba mtoto wao wa mwisho anapo mahala pa kukulia.

Uwezo kama naibu wa meya alikuwa nao na isitoshe, familia zao zote ziliwakubalia kwa kuwa mila zinaruhusu na jiko Zaidi la moja. Mambo yaliendelea kunoga hadi wakati uchaguzi mpya wa ugatuzi ulipozaliwa 2013.

Mchemko wa siasa ulianza kuchipuka kwa Aisha Jumwa na kuamua kujaribu bahati yake katika wadhifa mpya wa kiti cha mwakilishi wa kina mama. Kwanza, aliyekuwa mbunge wa Ganze, Francis Baya alikuwa amemuona kuwa mwanasiasa wa faida kutokana na uzoefu wake wa kuzungumza jukwaani na mipasho yake ya maneno.

Ingawahivyo, Karisa Nzai ambaye alikuwa bado yuko ngangari naye kama mume, alifanikiwa kuwarai viongozi wa jimbo wa chama cha ODM, hususan wa Mombasa na Kilifi kumuenzi Aisha Jumwa kwa tikiti ya chama katika kaunti ya Kilifi.

Maskini Karisa Nzai wakati huo hakujua kwamba alikuwa ameitafuta nyundo ya kukomelea msumari wa mwisho katika sanduku lao la mahaba.

Licha ya Nzai kuchaguliwa kama mwakilishi wa wadi ya Jomvu kwa tikiti ya ODM kwenye uchaguzi mkuu wa 2013, Jumwa alifanikiwa kuwa juu yake kwa kuchaguliwa kama mwanamke wa kwanza kuwakilisha kina mama wa kaunti ya Kilifi (2013-2017).

Na kweli kama wahenga walivyonena kuwa “Maskini siku akipata, makalio hulia mbwata”, kuchaguliwa kwa Aisha Jumwa ndio chanzo cha mapenzi ama ndoa yake na Karisa Nzai kuingia shari. Bwana mwakilishi wa wadi, mke mwakilishi wa kaunti nzima. Kwa kifupi, ilijitokeza sawa tofauti ya usiku na mchana.

Hata baada ya kuachana kwa sababu baada ya 2013, yasemekana kuwa mheshimiwa alianza Maisha yake mapya na hata kujenga ikulu yake Malindi katika maeneo ya Kakoneni, wadaku wanasema hakujakuwa na ngonjera kama ilivyokuwa kwa mume wake wa mwanzo.

Maisha mapya

Wachanganuzi wa masuala ya ndani wanasema kuwa Karisa Nzai aliamua kuendelea na maisha yake na akadinda kabisa kumkejeli Aisha kuhusiana na chochote kile alichomfanyia ama kumtolea kama mahari.

Wengine wanasema pia naye aliregeshewa marupurupu yake ya mahari na vimbuzi vyake kama ilivyokuwa kwa bwana wa kwanza.

Hatahivyo, familia yake ya karibu inasema kwamba Karisa Nzai hajaitisha wala kutaka chochote kutoka kwa mheshimiwa aliyeponyoka kwake kati ya miaka ya 2013 na 2014.

“Tulimshauri asichukue hatua yoyote kwa kuwa wote ni wazazi sasa wa msichana aliye kitimba mimba wa mheshimiwa Aisha Jumwa. Pia hatungependa mbunge wa Malindi kuzusha sarakasi ya kuregesha mahari kwake kama alivyomfanyia mumewe wa mwanzo,” mshauri mmoja wa upande wa Nzai alisema.

Sababu ya kuwa jina la Karisa limebakia kwenye majina rasmi ya mbunge huyu mcheshi, ni kwa sababu babake mzazi pia ni Karisa. Kabla ya mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa Karisa kuchaguliwa mwakilishi wa kina mama katika uchaguzi mkuu wa 2013, alikuwa Diwani na hata kuwa mwenyekiti wa baraza la wilaya ya Kilifi.

Tofauti ya maono

Wakati akiingia nyanja ya siasa angavu ya wilaya, mume wake wa kwanza kamwe hakufurahishwa na hatua ya Aisha Jumwa kujitosa uwanja wa siasa. Kulingana na taarifa zake za awali, yaaminika bwana huyu wa mwanzo alitofautiana akitete kwamba safu ya siasa haimfai mkewe.

Ndoto yake ilikuwa ni kujitosa kwenye siasa licha ya mumewe kukataa wazo hilo. Jumwa ambaye amezaliwa mtoto wan ne kutoka kwa Watoto 28 ijapo kutoka kwa mama tofauti, aliamua kuachana na mume wa kwanza ambaye pamoja na familia ya upande wa bwana huyo, ulikuwa ukimpinga vikali.

Ni bwana huyu wa kwanza ambaye Aisha Jumwa alimfungashia mahari yake kwa kuzichunga ng’ombe na mbuzi guu kwa guu hadi kwa chifu wa eneo lao kumregeshea mahari yake ili awe huru kisiasa isiyokuwa ya kero.

“Mume wangu aliniambia ikiwa nikubakia mwanasiasa mwaishani mwangu, nimlipe mahari yake. Nilimpeleka kwa naibu wa chifu kueleza nini anachodai kama mahari yake. Na kweli nilimlipa chote kile alichodai mbele ya chifu,” alinukuliwa Aisha Jumwa wakati mmoja na vyombo vya habari kuthibitisha hatua yake hiyo.