Licha ya serikali ya Kaunti ya Nairobi kutumia mabilioni ya fedha kwenye ujenzi wa barabara ili kupunguza msongamano wa magari jijini, wahudumu wa magari bado wanapitia changamoto si haba kuingia na kutoka jijini hali ambayo imesababisha hasara katika sekta ya uchukuzi.
Kwa mujibu wa washikadau katika sekta ya trafiki, uegeshaji wa magari katikati ya jiji unapaswa kupigwa marufuku na badala yake mabasi yanayobeba abiria wengi kutumika.
Aidha washikadau hao wamependekeza kupunguzwa kwa mizunguko jijini na badala yake kuongezwa kwa makutano ya barabara huku wakitoa mfano wa taifa ya Ujerumani ambapo magari yanaendeshwa bila uangalizi wa maafisa wa trafiki.
Hata hivyo wamehuzunishwa na mpangilio wa jiji kwa sasa wakisema polisi wanalazimika kuwa waangalifu wakati wote ili kuhakikisha usalama wa abiria barabarani.
Wakati uo huo, serikali ya Kaunti ya Nairobi imepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha barabara zinakarabatiwa, mabomba ya kupitisha maji-taka kuzibuliwa, kutoruhusu magari ya kuwabeba abiria kuingia katikati ya jiji miongoni mwa maswala mengine.
Washikadau hao wamezungumza jijini Nairobi muda mfupi uliopita.