Rais Uhuru Kenyatta amepinga vikali kuwa na uhusiano wowote na kampuni ya Uingereza ya Cambridge Analytica inayodaiwa kuednesha kampeni zake wakati wa uchaguzi wa mwaka 2013 na 2017.

Akihojiwa na shirika la habari la CNN, Rais amesema kuwa hana ufahamu wowote wa kushirikiana na kampuni hiyo kauli inayonekana kukinzana na matamshi na mmoja wa viongozi wa Jubilee David Murathe aliyesema kuwa walishirikiana na kampuni hiyo kubadilisha taswira ya chama hicho.

Ikumbukwe kwa mujibu wa kanda za video zilizopeperushwa katika makala ya ufichuzi na runinga ya Channel 4 News ya Uingereza, ilifuchuliwa kampuni hiyo kuwa ilihusika pakubwa katika kuhakikisha Chama cha Jubilee kinapata taswira mpya, kuandika hotuba za Rais Kenyatta pamoja na manifesto zake na kusambazwa kwa propaganda katika mitandao ya kijamii ambazo zililenga kumharibia sifa aliyekuwa mshindani wake mkuu, Raila Odinga.

Wakati wa mahojiano hayo, rais pia amesema kuwa taifa la Kenya halitilii maanani haki za watu walio na uhusiano wa jinsia moja kwani zinaenda kinyume na tamaduni za taifa hili na mataifa mengi ya Afrika.

Katika taswira sawa na ile iliyoshuhudiwa mwaka 2015 wakati wa ziara ya aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama, Rais Kenyatta amesema kuwa tamaduni za Kenya hazitambui suala la ushoga kuwa miongoni  mwa masuala muhimu ya taifa hili. Hata hivyo Rais amesema kikatiba kila mkenya ana haki na hakuna anayedhulumiwa wala kubaguliwa kutokana na hali yake ya kimapenzi.

Aidha amesisitiza kuwa kauli yake akiwa rais inawawakikilisha wakenya wote.