×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Tusikubali Jubilee ile watoto wetu jameni

News
 Nembo ya Jubilee Picha: Hisani

Musa aliwaokoa wafuasi wake kwa imani ya Mungu wake, dini yake na waliomfuata wakitanguliwa na imani ya Mungu wa Musa ili kuwaondoa katika utumwa.

Musa aliamini uwezo wa Mungu wake, hivyo basi uongozi wake na imani aliyonayo ukawa muhimu katika safari ile.

Lakin viongozi wa sasa hawajaiga nyayo za mitume, wala maandiko yake Mwenyezi Mungu. Viongozi wetu hawana tofauti na wezi wanaotuhangaisha kila kukicha kwa kutuibia kidogo tulichojaaliwa.

Matatizo yetu ni mengi, lakini tatizo kubwa zaidi ni kule kupoteza uhuru wetu — jambo ambalo limezaa viongozi wabovu ambao pia wamezaa ufisadi.

Kwa kweli tatizo kubwa tulilonalo kama jamii ni elimu ya uraia. Wananchi hawajui haki zao na jinsi ya kufuatilia haki zao zinapochukuliwa na viongozi au watu maarufu.

Hii inapelekea viongozi wetu kufanya watakavyo. Kenya ya sasa inaongozwa na watu walio na dhana ya kuwa kabila lao ndilo kabila la Musa — lililoteuliwa kuongoza wakenya.

Kenya ya sasa ni lazima uwe unatoka jamii fulani ndipo uwe mheshimiwa. Ni lazima uibe ukiwa katika jamii fulani ili uabudiwe.

Baka demokrasia, tukana wakenya wenzako kwa kuwapa majina ya ajaabu, maliza wanaokupinga, angamiza wanaoinuka kuuliza haki zao na juu hayo yote fanya Kenya kuwa mali yako. Hii ndio hali halisi ya Kenya ya sasa.

Leo — tofauti na makala yangu ya kila juma — nimeamua kuwa nyundo na kupiga msumari.

Nafahamu kuwa watu waliojawa ukabila watanichukia, wengi wanaoabudu miungu midogo watanilaani na kuniita kila aina ya majina. Hata hivyo, ukweli wa mambo ni kuwa katika serikali zilizopita, sijawahi ona serikali fisadi, hatari kwa usalama, dhalimu kama hii ya Jubilee.

Serikali inayomaliza Kenya na ukenya wetu.

Serikali ambayo imewapanda kichwa hata wanahabari na hivyo kuamua jinsi ya kuendesha mambo watakavyo — japo kimya kimya.

Kwa kifupi, serikali hii ni kila kitu. Ukitaka kuiba ambia serikali hii ikusaidie. Ukitaka ardhi tumia serikali hii. Ukitaka kujiondoa kwenye kesi hatari basi kula na serikali hii — kila kitu kitakuwa shwari.

Hii ni serikali inayoamini na kutumia demokrasia ya kijambazi kutawala wanyonge. Serikali inayotawala Kenya kwa msemo wa turihamwe au uthamaki.

Nembo ya kijinga inayowaunganisha wajinga wote wanaoamini rais Uhuru Kenyatta au ndugu William Ruto hulala njaa kama wao, hupata shida kama wao, hutembea kama wao kila alfajiri na macheo kabla jimbi halijameza punje na ardhi kupoteza umande.

Katika tawala hizi za uthamaki mfumo uliotumika kupata uongozi ni wa kurithishana madaraka. Yani, ikiwa mzazi ni mfalme, basi atakapofariki dunia, mmoja wa watoto wake ataridhi kiti cha ufalme cha baba yake.

Ukoo uliopata fursa ya kushika dola, ndiyo utaongoza siku zote na utatambulika kama ukoo wa kifalme. Katika kitabu chao cha uthamaki hapawezi kutokea kiongozi nje ya ukoo huo.

Huu ndio ukoo wa tangu na mwanzo wa hayati Mzee Jomo Kenyatta kumrithisha Daniel Moi, Moi na Kibaki kumrithisha Uhuru Kenyatta na Uhuru Kenyatta kumrithisha uthamaki mwingine atakayefuata nyayo hizo hizo na kuonekana kama mwana-uthamaki.

William Ruto hajatokea ukoo wa uthamaki, na kama bado ana ndoto ya kurithishwa, ole wake.

Ruto ametokea ukoo wa kuuza kuku na kutumia kifua ili kuishi. Ukoo wa kujisaidia. Najua Ruto anafahamu haya na anajua wazi kuwa ndoa yao itafikia ukingoni pindi tu Uhuru Kenyatta atajishinda awamu ya pili.

Awamu ya ndoto tasa ya uongozi.

Yao hata haikuwa ndoa bali ilikuwa ni mapenzi ya kusaidiana kujiondoa katika kesi ya mahakama ya jina huko Hague. Kenya inaweza kuwa ndio nchi pekee katika Afrika na pengine duniani, yenye idadi kubwa ya viongozi wa kisiasa ambao ni waongo na wanafiki.

Viongozi wasiowajali na walevi wa uongozi kupindukia. Leo naona vugu vugu la tatu likianza kwa kasi kukomboa taifa hili, leo naona vijana waliochoshwa na uongozi wa ki-imla wakidai haki zao.

Leo natabasamu maana naona vijana kama Boniface Mwangi wakisimama imara na kuwakosoa wanaojiona jabali.

Leo naona safari ya kurudisha hadhi ya Ikulu ya Nairobi ikianza kwa kishindo. Safari ya kuwaondoa wezi wote Kenya. Wananchi wanafaa wafanye maamuzi magumu ya kuwakataa viongozi waongo na wafisadi.

Kataeni kuuawa kwa watoto wenu, kataaeni wizi wa mali ya umma, kataeni wizi wa ardhi, kataeni mauaji ya kiholela, kataeni ukosefu wa ajira, kataeni demokrasia ya kijambazi, kataeni ukabila, kataeni kutawaliwa na miungu watu, kataeni wizi wa kura na juu ya hayo yote kataeni kuchaguliwa viongozi na watu fulani chini ya nembo wa UTHAMAKI!

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles