Mawakili waandamana kulalamikia kutoweka kwa mmoja wao

Hisia zinazidi kuibuliwa kufuatia kutekwa nyara kwa wakili Willie Kimani na wateja wake wawili siku kadhaa zilizopita. Mawakili jijini Nairobi wamefanya maandamano huku wakishinikiza kuhusishwa katika uchunguzi wa kisa hicho.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tawi la Nairobi Charles Kanjama, mawakili hao wametoa makataa ya siku saba kwa idara zinazohusika kutoa ripoti kamili kuhusu kutekwa nyara kwa wakili huyo.
Hayo yanajiri huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiongozwa na Shirika la KNHCR, yakisema kuna njama ya serikali kuwahangaisha watetezi wa haki za binadamu nchini.
Kwenye kikao na wanahabari leo hii Kamishna wa KNHCR Partricia Nyaundi, amesema iwapo idara hizo hazitatoa ripoti kuhusu waliko mateka hao ifikiapo mwishoni mwa wiki hii, watalazimika kuchukua hatua nyingine kukiwamo kuwasilisha kesi mahakamani.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Makueni, Daniel Maanzo amesema huenda wakalazimika kuwasilisha ombi kumshinikiza Wazi  ri wa Masuala ya Ndani ya Nchi Joseph Nkaisery kufika mbele ya kamati za bunge kutoa maelezo kufuatia mienendo ya maafisa wa polisi wanaodaiwa kutekeleza kitendo hicho.
Wakili Kimani Wateja wake Joseph Muiruri na Josphat Mwenda wanasemekana kutekwa nyara na maafisa wa polisi wa utawala AP tarehe 23 mwezi huu na hawajulikanani waliko hadi sasa.
Na, Carren Omae

Related Topics