Utendakazi wa Jopo la Kumchunguza Jaji Tunoi Wafikia Kikomo

Jopo lililokuwa likichunguza madai ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Juu Philip Tunoi litalazimika kuwasilisha ripoti yake ya uchunguzi bila mapendekezo kuhusu uchunguzi uliofanywa dhidi yake.
Mwenyekiti wa jopo hilo, Sharad Rao amesema hali hiyo imetokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu iliyodumisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wa kustaafu kwa majaji wakiwa na umri wa miaka sabini. Jopo hilo lina mamlaka ya kumchunguza jaji anayehudumu pekee. Kustaafishwa kwa Jaji Tunoi baada ya kufikisha umri wa miaka sabini na miwili kunamaanisha kwamba jopo lililokuwa likimchunguza halitaendelea tena na vikao hivyo.   
Kupitia wakili wake Fred Ngatia, Tunoi amekubali uamuzi wa kusitishwa kwa vikao hivyo. Awali, alitaka jopo hilo liendeleze vikao vyenyewe hadi tamati ili kumwondolea tope la kuhusishwa na tuhuma za kupokea hongo.
Mlalamishi Geoffrey Kiplagat alidai kuwa Tunoi alipokea hongo ya shilingi milioni 200 kutoka kwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero ili kushawishi uamuzi kwenye kesi iliyopinga kuchaguliwa kwa Kidero kuwa Gavana wa Nairobi.

Na, Beatrice Maganga

 

Related Topics

philip tunoi